Clarende Seedorf adai hana wasiwasi wa kutimuliwa kazi AC Milan
Aliyekua kiungo kutoka nchini Uholanzi Clarence Seedorf ameonyesha kujiamini katika kazi yake huko mjini Milan baada ya kikosi cha klabu anayoinoa kwa sasa AC Milan kukubali kipigo cha mabao manne kwa mawili mbele ya AS Roma.
Clarence Seedorf ameonyesha kujiamini huko, kufuatia kauli aliyoitoa mbele ya vyombo vya habari kwa kudai hana wasiwasi na suala la kutimuliwa kazi kwenye klabu hiyo, kutokana na kuamini klabu ya AC Milan inaweza kumpatia kazi nyingine ya kufanya.
Seedorf amesema huenda mashabiki wa klabu ya AC Milan wakawa na mawazo ya namna hiyo, lakini kwake anaamini uongozi unatambua mchango alioutoa ndani ya klabu hiyo tangu alipoanza kuitumikia mwaka 2002 kama mchezaji.
Amesema kufungwa ni sehemu ya mchezo, licha ya kikosi chake kushindwa kufanya vyema katika michezo mitatu mfululizo, lakini bado anaamini matokeo hayo sio mwisho wa malengo waliyokubaliana na viongozi wa AC Milan ambao aliingia nao mkataba mwanzoni mwa mwaka huu.
Hata hivyo Clarence Seedorf amesisiza jambo la ushirikiano kuendelea kudumishwa kati yake na watu wa karibu na klabu ya AC Milan kwa malengo ya kukamilisha maazimio anayoyakusudia hadi mwishoni mwa msimu huu.
Katika hatua nyingine Seedorf ameonyesha kutokuwa na matumaini na msimu huu kwa kuamini tayari kikosi chake kimeshashindwa na hivyo amekiri kuanza kupanga mikakati kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.
Kupoteza mchezo wa jana kwa kukubali kufungwa mabao manne kwa mawili dhidi ya AS Roma kunaifanya AC Milan kuendelea kubaki katika nafasi ya kumi na moja kwenye msimamo wa ligi ya nchini Italia, na hivyo kuhatarisha historia ya klabu hiyo kongwe kushiriki michuano ya barani Ulaya.
No comments