Gerardo Martino asema bado hajafanya maamuzi sahihi ya kikosi cha Barcelona mechi ijayo.
Baada ya ushindi wa mabao saba kwa sifuri dhidi ya Osasuna, meneja wa klabu ya FC BarcelonaGerardo Martino amesema bado hajafanya maamuzi sahihi ya kukipanga kikosi chake kwa ajili ya mchezo ujao wa ligi ambapo watapambana na mahasimu wao Real Madrid kwenye uwanja wa Stantiago Bernabeu.
Gerardo Martino ametangaza matarajio ya kukipanga kikosi chake kuelekea kwenye mchezo dhidi ya Real Madrid, kutokana na kutambua umuhimu wa mchezo huo, ambao hukabiliwa na changamoto kadhaa kutoka kwa wachezaji hadi kwa mashabiki wa klabu hizo mbili.
Martino amesema maamuzi ambayo atayachukua ya kuamua nani anastahili kuanza katika mchezo huo, yatatokana na mwenendo wa wachezaji wake katika siku zilizosalia, huku akiamini kila mchezaji wake ana uwezo wa kucheza mchezo huo.
Amesema tangu alipoanza kukinoa kikosi cha FC Barcelona mwanzoni mwa msimu huu amekua akionyesha kumuamini kila mchezaji wake kikosini, hivyo hatopanga kikosi kwa kutazama jina la mchezaji fulani na kumuacha mwingine.
Hata hivyo meneja huyo kutoka nchini Argentina ameonyesha kuwaheshimu sana Real Madrid kwa kusema ni klabu ambayo imeonyesha dhamira ya kuhitaji mafanikio msimu huu, hivyo watakwenda kwa tahadhari kubwa, huku akiwaamini wachezaji wake.
Wababe hao wa soka nchini Hispania wanajiandaa kupambana mwishoni mwa juma hili, huku Real Madrid wakiwa kileleni mwa msimamo wa ligi ya nchini humo kwa kufikisha point 70, ambazo ni tofauti ya point nne dhidi ya FC Barcelona wenye point 66 ambazo zinawaweka kwenye nafasi ya tatu, wakitanguliwa na Atletico Madrid wenye point 67
No comments