Monalisa amesema waigizaji wengi Tanzania hukosa sapoti wanapowania tuzo kubwa Afrika, kwasababu ma-director huangalia uzuri kuchagua wahusika.
Muigizaji anaetajwa kuwa kati ya waigizaji bora zaidi wa kike katika filamu za kitanzania, Yvonne Cherryl aka Monalisa ameeleza kuwa waigizaji wa Tanzania hushindwa kung’ara wanapotajwa kuwania tuzo kubwa Afrika kwa kukosa sapoti ya Watanzania.
Nyota huyo wa filamu ya Siri ya mtungi ameeleza katika makala iliyoandaliwa na Rahab Fred wa 100.5 Times Fm iliyokuwa ikielezea juu ya ushindi wa wa Mkenya Lupita Nyong’o kama mfano wa kuigwa kwa waigizaji na wadau wa filamu Tanzania.
Monalisa alieleza kuwa Lupita amefanikisha kutokana na sapoti kubwa aliyoipata kutoka kwa wakenya tangu awali, na kutoa mfano wake na tamthilia ya ‘Siri ya Mtungi’ kuonesha jinsi watanzania wasivyosapoti vya kwao.
“Kwa watanzania nikisema eti watu wote kwa ujumla tumpush mtu yaani hiyo ntahubiri mpaka mwaka kesho. Kwa sababu kuna watu kibao…mimi mwenyewe niliwahi kuwa nominated kwenye tuzo za Nigeria lakini zinafanyika New York kila mwaka. Nilikuwa nominated na nilikuwa msanii wa kwanza kwa wakati huo. Niliomba kura lakini hamna mtu ambaye alijitolea kusema kwamba labda jamani tumpigie kura huyu ni mtanzania mwenzetu. Lakini wanakusubiri mpaka ufike kwenye mafanikio ndio wanaanza kusema kuwa huyu ni wa kwetu jamani tumpigie kura.” Alisema Monalisa.
Aliongeza kuwa ingawa tamthilia ya ‘Siri ya Mtungi’ ilikuwa nominated kwenye vipengele 7 kwenye tuzo za AfricaMagic Viewers Choice Awards mwaka huu, na Juma Rajab aka Cheche akitajwa katika kipengele kimojawapo, hakuna hata msanii mmoja aliyepost kumuombea kura.
Katika hatua nyingine, Monalisa aLiwashauri wasanii wa Tanzania wasibweteke wanapopata nafasi ya kuingia kwenye tasnia ya filamu bali waongeze jitihada, kusoma na kufuatilia kwa ukaribu weledi wa mambo ya filamu. Alidai kubweteka kunachangiwa na tabia ya baadhi ya ma-director kuangalia uzuri wa msichana kama kigezo cha kuwapata washiriki kabla ya uwezo wa kuigiza.
“Unajua wasanii wa Bongo wengi wanachukuliwa labda hivi director amepita amemuona msichana mzuri, wenyewe siku hizi wakiona msichana mzuri wanasema ‘cast ile’. Kwa hiyo mtu anachukuliwa tu akishajiona ‘ah mimi ni mzuri nikishavaa kimini changu hapa nauza’, basi anajibweteka hafanyi chochote kuhusiana na kazi yake..”
Tamthilia ya Siri ya Mtungi, ilitajwa kuwania vipengele saba katika tuzo za AMVCA 2014 zilizofanyika jana jijini Lagos, Nigeria, lakini iliambulia patupu.
No comments