HATIMAYE LULU AACHIWA NJE KWA DHAMANA "ALWAYS GOD IS GREAT"

Mahakama kuu leo imetangaza dhamana ya mwigizaji Lulu lakini iwapo atatimiza masharti aliyopangiwa ambayo ni pamoja na kuwasilisha hati yake ya kusafiria, kutosafiri nje ya Dar es salaam, kujiwakilisha au kuripoti mahakamani kila siku ya kwanza ya kila mwezi pamoja na wadhamini wake wawili ambao kila mmoja adhamini kwa shilingi milioni 20 za kitanzania.
Upande wa familia ya Lulu umesema masharti yote yaliyotajwa wanaweza kuyatimiza leo leo hivyo wanasubiri tu jibu la msajili ambae ndio anatakiwa kuhakikisha hayo masharti yametimia kisha ruhusa ya kumkabidhi Lulu kwa familia yake itolewe.
Taarifa za ndani ni kwamba uwezekano wa Lulu kuachiwa upo kuanzia january 29 2013 ambayo ni kesho kwa sababu kuna watumishi wawili wa serikali ambao wapo kikazi mkoani Pwani na ndio walitakiwa kutia saini dhamana ya Lulu wakiwa ni sehemu ya masharti.
Kwa wiki kadhaa sasa, baadhi ya watu wamekuwa
wakisikika wakiomba dua njema kwa msanii huyo ili aweze kuachiwa kwa dhamana na kufuatilia kesi yake akiwa nje na familia yake. Lulu aliwasilisha mahakamani hapo maombi ya dhamana, kupitia kwa jopo la mawakili wake, linaloongozwa na Wakili Kennedy Fungamtama, Peter Kibatala, Fulgence Masawe wa Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Awali, maombi hayo ya dhamana yaliwasilishwa mahakamani hapo kwa hati ya dharura na kusikilizwa na jaji Zainabu Muruke.
Mara baada ya tukio la mauaji ya Kanumba kutokea, kesi ya msanii huyo ilifunguliwa katika Mahakama ya Kisutu ili kukamilisha hatua za awali, hasa masuala yote ya kisheria, upelelezi na kushtakiwa kwa mauaji ya kuua bila kukusudia kwa kupitia Kifungi cha 196.
Kesi ya Lulu yenye namba 125, jalada lake lilifungwa na kuhamishiwa Mahakama Kuu kwa kuwa ndiyo yenye uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji.
Mara baada ya kufika mahakamani hapa leo asubuhi, dalili njema za kuachiwa kwa msanii zilianza kujitokeza hasa baada ya dhamana yake kuwa wazi, ikiwa ni kutokana na hoja zilizokuwa zinajadiliwa mahakamani hapo.
Katika mitandao ya kijamii, ikiwamo facebook, baadhi ya watu walionekana wakipost habari na picha mbalimbali za msanii huyo zikionyesha dhahiri kumuombea mema ili atoke na kuendelea na maisha yake wakati kesi hiyo inaendelea.
Lulu ni miongoni mwa wasanii wa kike wenye mvuto mkubwa katika jamii, huku uwezo wake na umahiri wake wa uigizaji ukiacha watu midomo wazi.
Umaarufu wa Lulu ulitokea tangu mdogo akiigiza katika kundi la Kaole Sanaa Group, akicheza kama mt0to hadi kufikia kuwa msichana na mwenye mvuto miongoni mwa mabinti wa filamu Tanzania.
Bila shaka habari za kuachiwa kwa dhamana kwa msanii huyo zitakuwa njema kwa siku ya leo kwa mashabiki na wadau wote wa filamu Tanzania.
Unaweza kumsikiliza mwigizaji Dr Cheni hapo chini, ni mmoja ya watu waliokaribu na familia ya Lulu na ameshirikiana nayo kwa muda mrefu sana kwenye hii kesi ikiwemo kufatilia mawakili, kushughulikia dhamana na mengineyo.
No comments